Maana ya falsafa ya kiafrika kwa mujibu wa Placide Tempels, Falsafa ya
kiafrika ni ile falsafa inayowashughulisha waafrika wenyewe na watu wengine
ambao sio waafrika lakini wanakubaliana na mila, tamaduni za waafrika na fasihi
simulizi za kiafrika.Hivyo falsafa ya kiafrika ni ile falsafa ambayo imejikita
katika mifumo ya kijamii, mila na desturi na fasihi simulizi za kiafrika.
Placide Tempels alizaliwa tarehe 18/02/1906 katika mji wa Barcal huko
Ubelgiji na alikufa tarehe 09/10/1977 akiwa na umri wa miaka sabini na moja
huko huko Ubelgiji. Aliishi Kongo kwa miaka ishirini na tisa mpaka pale
aliporejea kwao ubelgiji. Kwa kipindi
chote alipokuwa Kongo alifanya kazi kuu mbili, kazi ya umishenari na uandishi.Katika
kipindi chote hicho alichokaa Kongo alisoma tabia ya waafrika wanaoishi Kongo
hususani kabila la Waruba, na akabaini kuwa waafrika wana tamaduni zao
zilizojikita katika fasihi simulizi. Hivyo akaandika kitabu chake kiitwacho “The Bantu philosophy” (1945), katika
kitabu hicho anapinga mawazo ya wazungu kwa kusema kuwa waafrika wanafalsafa
yao na hivyo Tempels akatumia hoja kadhaa kutetea mawazo yake hayo, kama imani
ya uchawi, hofu ya uhai na kifo, nguvu hai, suala la ndoa na dhana ya uduara.
Katika kujibu swali hili riwaya ya “Mirathi
ya Hatari” ndio inayotumika. “Mirathi
ya Hatari” ni riwaya ilioandikwa na C. G. Mung’ong’o (1977). Riwaya hii
inajaribu kuelezea visa na mikasa ya kisihiri iliojitokeza katika jamii za
kiafrika hususani katika jamii ya Njombe (Kiterevadzi) na maeneo mengine. Hivyo
msanii amemtumia mhusika Gusto ambaye ndiye anayerithishwa mirathi ya hatari
kutoka kwa baba yake Mzee Kazembe, mirathi hiyo ndiyo inayopelekea vifo vingi
kutokea ikiwemo visasi mfano kifo cha mama yake Gusto na dada yake Nandi, pia
inapelekea kifo cha mjomba ake Gusto Kapedzile. Ukiachana na vifo hivyo pia
inapelekea kutokea kwa matukio mengi ya kiuchawi.
Ufuatao ni uhakiki wa riwaya ya “Mirathi
ya hatari” kwa kuzingatia misingi ya kisalsafa kama ilivyoainishwa na
Placide Tempels katika kitabu cha “The
Bantu Philosophy” na kuonyesha uhalisia wake na faida na hasara ya falsafa
hiyo katika jamii ya kitanzania.
Imani ya uchawi, Katika falsafa ya imani ya uchawi Tempels anaamini kwamba
waafrika wanategemea sana nguvu za kichawi, katika kuelezea suala hilo Tempels
anajaribu kuangalia jamii ya Ulaya kwamba wengi wapatapo matatizo hurudi kwa Kristo
lakini jamii nyingi za Afrika pindi wapatapo matatizo hutegemea uchawi kama suluhisho
la matatizo yao wanayarudisha kwenye imani za kishirikina. Falsafa hii ya imani
ya uchawi imejitokeza kwa kiasi kikubwa sana katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari” kwani kuna matukio
mengi ambayo yanadhihirisha hilo. Mfano, kitendo cha Gusto kukabidhiwa mirathi ya
uchawi kutoka kwa baba yake. Mfano uk. 15 Mzee Kazembe anamwambia Gusto
“Mwanangu nakuachia kazi kubwa. Ni urithi mkubwa ukiutumia vyema, bali pia ni
mirathi ya hatari usipojihadhari nayo, nakuachia dawa zote za milki yangu
katika mizungu ya sihiri”. Pia uwepo wa kiapo cha uchawi, unadhihilika pale
ambapo Gusto anaapishwa kama ni uaminifu wa kuingia katika uchawi kiapo hicho
kila mtu anahitaji kiapo ndipo awe mchawi; mfano katika ukurasa wa 21
anaonekana akiapa kwa kutamka maneno, “Enyi Mahoka na Mababu...”. Pia mazingira
ya vifo vyote, vinatokea katika mazingira ya utatanishi ambayo ni mazingira ya
kichawi. Mfano, kifo cha Kapedzile, ambaye aliuliwa na Gusto, kifo cha Dina
ambaye aliuliwa katika mazingira ya kichawi na baba yake, kifo cha mama yake
Gusto Nyamidze na Nandi ambao walikuwa na Malipula kwa kutaka kulipa kisasi na
kifo cha Malipula aliyeuliwa na Gusto pamoja na Mavengi katika mazingira ya
Kichawi.
Katika jamii yetu ya kitanzania imani ya uchawi inajitokeza sana kwani kuna
matukio mengi yanayojitokeza na yanaonekana kiuhalisia mfano watu kugandishwa
katika nyumba za watu na pia kila kukicha wanaonekana wakianguka usiku na
Nyungo zao, pia suala la uwepo wa misukule katika nyumba za watu. Pia baadhi ya
watu kutumia hirizi kama kinga. Falsafa ya imani ya kichawi haina nafasi katika
jamii kwani inasababisha migogoro mingi, maafa pamoja na kurudisha maendeleo
nyuma. Hivyo wanajamii wa leo wanaaswa kuachana na imani za kichawi.
Hofu ya uhai na kifo. Hii ni hoja nyingine ya Tempels kwani anaamini kuwa Waafrika
wana hofu ya uhai na kifo. Kwa kudhihilisha hili anaweza kuangalia salamu zao,
na pia mtu anapopatwa na ugonjwa anaamini hawezi kupona na kifo kinamsogelea. Wazo
hili limejitokeza pia katika riwaya ya “Mirathi
ya Hatari” mfano pale Mzee Kazembe anapomueleza mwanae kuwa hali yake ni
mbaya na kifo kinamkaribia uk. 15 “Siku zangu zimekwisha sidhani kama nitaishi
zaidi”. Pia mama yake Gusto alikuwa na hofu na uhai wa Gusto na ndio maana
akamuusia aachane na mirathi aliyokabidhiwa na baba yake kwani anaweza
akapoteza maisha. uk 38 “Sipendi nimpoteze tena hata mmoja wenu kabla sijafa”.Pia
suala la salamu na kujua hali ya mtu inaonesha hofu ya kifo, mfano ni pale
Malipula alipokwenda nyumbani kwa kina Gusto walianza kujuliana hali uk. 57,......Nikawauliza.....,
“Habari za nyumbani wazee wangu”, “Nyumbani kwema tu” alijibu mzee Kindimba
“Lakini hatujui ya huko nyuma”
Suala la hofu ya uhai na kifo linajitokeza sana katika jamii ya kitanzania
mfano, Watanzania asubuhi wakiamka au wasipoonana muda mrefu basi hutoleana
salamu na kujuliana hali, pia pale mtu anapoamua watu huwa na wasiwasi sana na
uhai wake hivyo hujikithirisha
kumuombea dua ili aweze kupona. Falsafa ya uhai na kifo ina nafasi katika jamii
kwani inawafanya wanajamii kuchukuwa tahadhari ili kuzuia kifo, pia inaendeleza
dhana ya kustawisha zaidi uhai. Kwa upande mwingine falsafa hii in hasara kwani
hurudisha nyuma maendeleo kwa sababu mtu ataogopa kufanya suala la maendeleo
kwa kuhofia kifo ambacho kitamfanya kuacha mali zote alizochuma pia kutotimiza
malengo yake.
Waafrika wanaamini katika suala la ndoa, pia hili ni wazo la Placide Tempels
ambae anasema kuwa waafrika wanaamini sana katika ndoa zao na ndoa hizo
hudumishwa ili kupata watoto. Uhai wa binadamu unaanzia kwenye mimba ambayo ni
matokeo ya Ndoa. Wazo hili linaonekana sana katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari” mfano ndoa ya Kazembe
na Nyamidze watoto wanaopatikana ni nane na wanaokufa ni watoto watano ambapo
uk. 5 unaonyesha hilo. Pia familia ya
Malipula na mkewe pia wana watoto. Pia mjomba wake Dina alikuwa na ndoa
iliyompeleka kupata watoto katika uk.78.
Suala hili la ndoa linasawiri maisha halisi ya kila siku ya Tanzania mfano
kuna ndoa za kanisani, msikitini ndoa za serikali na ndoa za kijadi. Suala la
ndoa lina nafasi kubwa katika jamii kwani inaendeleza nguvu kazi inayotokana na
watoto wanaozaliwa ambao wanatumika katika ujenzi wa taifa kwa sababu
hujishughulisha na shughulu mbalimbali
za ujenzi wa taifa. Pia falsafa hii huunganisha jamii, vile vile inaleta
heshima katika jamii. Kwa upande wa hasara ni pale inapotokea ndoa za
kulazimishwa au umri mdogo, kwani kuna wazazi wanawazoesha watoto wao wakiwa
bado wanafunzi.
Waafrika wanaamini katika nguvu hai, hili ni wazo jingine la Tempels kwani
anasema kwamba waafrika wanaamini sana katika nguvu hai na wanaamini kwamba
chanzo kikuu cha nguvu hai ni Mungu mwenyewe, nguvu hii hupitia kwa wahenga nao
hupeleka kwa mizimu ambao hupeleka kwa binadamu na binadamu hupeleka kwa
wanyama na mimea. Tempels anasema waafrika wanaamini nguvu ya waganga na hivyo
mganga ana uwezo mkubwa wa kupunguza au wakuongeza nguvu hai kwa binadamu. Tempels
anajiuliza maswali kadhaa kuhusiana na suala la waganga mfano, Dawa zawezaje
kuponya?, Dawa inawezaje kuua mtu aliye mbali?, ni vipi mtu aliyekufa anaweza
kuzaliwa upya?,na anasema kitendo cha kupungukiwa nguvu huitwa “Kufwa” na
“Kufudwilika” katika ukurasa wa 22. Hivyo Tempels anasema kuwa majibu ya
maswali yote matatu, ili uweze kujibu maswali hayo ni lazima uwe mshirika wa
mambo hayo. Dhana hii inajitokeza katika riwaya ya “Mirathi
ya Hatari” mfano baada ya kufa Mzee Kazembe mke wake Nyamidze alikwenda kwa
mganga kuthibitisha nini hasa chanzo cha kifo hicho uk.37. “Mwanangu leo
asubuhi nilikwenda kwa mama Tamwene kuulizia kifo cha baba yako. Mganga anasema
kuwa kifo chake kimetokea si kwa mapenzi ya Mungu ila kwa michezo ya binadamu
wafaidio kuwaona watu wakifa” Mama Gusto alimwambia mwanawe Gusto. Pia Malipula
alitaka ampeleke Gusto kwa Chikanga (Mganga) ili kubaini kama amehusika na mauaji ya Kapedzile katika uk.60.
Jambo hili katika jamii ya sasa bado linaendelea, kwani Watanzania wengi
huenda kwa waganga ili kukamilisha mambo yao, mfano kwenye masuala ya siasa,
elimu, biashara, kilimo, mauaji ya albino, upigaji wa nondo, uchunaji wa ngozi
yote haya yanahusishwa na waganga. Falsafa hii ina nafasi katika jamii kwani
inaendeleza uhai pale mwanadamu anapojihangaisha na kutafuta tiba ya maradhi
yake na hatimae anaweza kupona na kuendelea kuishi. Pia imani hii ya ya nguvu
hai inaweza kupelekea migogoro katika jamii hasa waganga wa jadi
wanaposhirikishwa katika kuongeza nguvu hata pamoja na kupiga ramli huzusha
mgogoro katika jamii.
Dhana ya uduara, katika wazo hili Tempels anasema kuwa waafrika hupenda
vitu vya umbo la uduara kwani wanaamini kuwa hivyo ndivyo vitu vizuri. Mfano
katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari”
dhana hii inaonekana sehemu nyingi. Mfano, pale Gusto alipoingizwa kwenye pango
na kukalishwa katika kigoda chenye umbo la duara katika ukurasa wa 33. Pia
Gusto anapomsifia Dina kuwa ana uso wa mviringo katika ukurasa wa 30. Vile vile
Mavengi anapoupitisha mgwisho wake na kuwazungushia Dina na Gusto katika umbo
la duara uk.73. Hata meza ya Gusto ilikuwa ni ya mviringo.
Dhana hii inajitokeza katika jamii ya leo mfano nyumba za msonge katika
kanda ya ziwa, Mikao ya kula huwa katika duara pia vyombo vingi huwa na umbo la
duara kama sufuria ,Vyungu, Vinu, Nyungo za kupepetea na Ngoma. Falsafa ya
uduara ina nafasi katika jamii kwani hudumisha na kuendeleza utamaduni wa
mwafrika, kwani tangu zamani inaaminika kuwa kila kitu chenye uduara ni kizuri,
pia kuna jamii nyingine zinazoendeleza kujenga nyumba za msonge. Hasara ya
falsafa hii hushirikisha imani hii ya uduara kama ndiyo kitu pekee kizuri,
kwani kuna vitu vingine ambavyo si duara na ni vizuri.
Kwa ujumla Placide Tempels ametoa mchango mkubwa sana juu ya falsafa ya
kiafrika, ambaye anakubali kabisa kuwa waafrika wana falsafa yao. Mawazo yake
yanapelekea kuibuka kwa wanafalsafa wengine wanaoizungumzia falsafa ya kiafrika
kama vile Kwame Nkurumah, J. K. Nyerere, Kenneth Kaunda. Hivyo basi mawazo yake
yana uhalisia pia yana umuhimu katika jamii ya kiafrika.
MAREJEO
Mung’ong’o C. G.
(1977), Mirathi ya Hatari. Dar es
salaam: Tanzania Publisha House.
Tempels, P, (1959),The Bantu Philosophy. Paris: Presence
Africaine.
Kazi nzuri
ReplyDeleteGreater work
ReplyDelete