Showing posts with label Kiswahili. Show all posts
Showing posts with label Kiswahili. Show all posts

Wednesday, May 7, 2014

Abiri data ifuatayo ya kiitariano kasha ubainishe yafuatayo:

Abiri data ifuatayo ya kiitariano kasha ubainishe yafuatayo:-
a.       [tinta]-rangi
b.      [ntɛnda]-hima
c.       [ntɛrɔ]-nyeusi
d.      [sapɔndɛ]- sabuni
e.       [tiŋgɔ]- napaka rangi
f.       [fuŋgɔ]- uyoga
g.      [tɛŋgɔ]- uyoga
h.      [bJaŋka]-nyeusi
i.        [faŋgɔ]- matope
j.        [ɑŋkɛ]

       I.            Je kuna jozi linganuo finyu? Ni hitimisho gani unalolitoa kuhusu jozi hizo?
    II.            Ni kigezo kipi kinahusika na mtawanyo wa sauti [n] na [ŋ] katika data hii?
 III.            Je sauti [n] na [ŋ] ni alofani za fonimu moja au ni fonimu mbili tofauti?
 IV.            Je kuna kanuni yoyote inayoshika mtawanyo huo?


 **************










                                i.            Je kuna jozi linganuo finyu?

Ndiyo ipo jozi linganuo finyu kwa sababu kama anavyosema Fischer (1957) anaeleza kuwa jozi linganuo finyu ni tofauti ndogo kabisa ya kifonolojia iliyopo baina ya maneno fulani Aghalabu maneno hayo huwa yana: Idadi sawa ya fonimu, mpangilio sawa wa fonimu ila unatofautishwa na fonimu mbili ambazo zipo katika mazingira sawa ya utokeaji.

Hivyo kutokana na data tuliopewa kuna maneno yenye idadi sawa na mpangilio sawa wa fonimu. Maneno hayo ni:-
[tiŋgɔ] na [fuŋgɔ]
[tɛŋgɔ]     [faŋgɔ]

Hitimisho tunalotoa katika jozi hizi ni kwamba katika lugha ya kiitaliano maneno haya [tiŋgɔ], [tɛŋgɔ], [fuŋgɔ] na [faŋgɔ] yana idadi sawa ya fonimu na mpangilio sawa wa fonimu ila tofauti kidogo inayojitokeza katika fonimu [i], [ɛ], [u] na [a].

                              ii.            Ni kigezo kipi kinachohusika na mtawanyo wa sauti [n] na [ŋ] katika data hii?

Kuna vigezo viwili vinavyohusika na mtawanyo wa sauti [n] na [ŋ] vigezo hivyo ni mgawanyo wa kimtoano na ufanano wa utofauti wa kifonetiki.
Mgawanyo wa kimtoano ni dhana ambayo hutumiwa kuelezea uhusiano uliopo baina ya sauti mbili au zaidi ambazo haziwezi kutokea katika mazingira sawa, kama ilivyo katika maneno ya kiitariano katika data, [tɛŋgɔ], [tiŋgɔ], [fuŋgɔ] na [faŋgɔ]. Mahali inapotokea sauti[n], sauti [ŋ] haiwezi kujitokeza.
Mfanano wa kifonetiki ni sauti zinazofanana kifonetiki au ni sauti zilizo na sifa bainifu zinazofanana. Kama ilivyo kwa [tinta], [ntɛnda], [ntɛrɔ] katika data ya kiitaliano.

                            iii.            Sauti [n] na [ŋ] ni alofoni za fonimo moja au fonimu mbili tofauti?

Sauti [n] na [ŋ] ni alofoni za fonimu moja kwa sababu Mgullu (1999) anasema Alofoni ni matamshi tofauti tofauti ya fonimu moja. Kwa asili neno hili ni la kigiriki Alo- ni tofauti tofauti na Foni -ni sauti.

Kwahiyo alofoni za sauti moja huunda kundi moja ambazo hubadili maana ya maneno. Alofoni zote hufanana kisauti. Na mofimu ni kipashio kidogo katika lugha ambacho kina sifa pambanuzi za kuweza kutofautisha vipande vingine vya aina yake (Massamba 2004).

Hivyo sauti [n] na [ŋ] ni alofoni za fonimu moja kwa sababu tunaona kuwa nazali /n/ inapofuatiwa na kitamkwa /d/ na /t/ hubakia kuwa /n/. Pia nazali /n/ inapofuatiwa na kitamkwa /g/ hubadilika na kuwa [ŋ]. Hivyo hii ina maana kuwa katika mazingira haya sauti /n/ na /ŋ/ ni alofoni za fonimu jumuishi /N/ kwa mfano:-
[tiŋgɔ], [tɛŋgɔ], [fuŋgɔ] na [faŋgɔ].

                            iv.            Je kuna kanuni yoyote inayoshika mtawanyo huo?

Ndiyo kuna kanuni inaoshika mtawanyo huu.
/N/→[α mahali]/-k
Kwa kuhitimisha tumeona kuna jozi linganuo finyu kama tulivyoona kwenye data ya [tiŋgɔ], [tɛŋgɔ], [fuŋgɔ] na [faŋgɔ], vile vile tumeona kuna vigezo vya ufanano na utofauti wa kifonetiki na mgawanyo wa kumtoano na fomula inayoshika mtawanyo huo ni:-
/N/→[α mahali]/-k







MAREJEO
Massamba, D.P.B na Wenzake (2009), Fonologia ya kiswahili sanifu
           ( Fokisa),sekondari na vyuo,Taasisi ya uchunguzi wa
                              kiswahili: Chuokikuu cha Dar es salaam.
Mgullu R.S (1999),Mtaala wa isimu, fonetiki, fonolojia na mofolojia ya kiswahili: Longman publishers(Kenya) Ltd.

Ulinganishi na ulinganuo wa hadithi fupi andishi na rwaya za kiswahili.




Wataalamu mbalimbali wametoa fasili mbalimbali za hadithi fupi andishi kama ifuatavyo:-
Msokile (1992) Anasema, hadithi fupi ni aina ya kazi ya sanaa ya utanzu wa hadithi inayotumia lugha iliyoandikwa katika nathari au iliyo katika masimulizi kama haijaandikwa. Ni wazi kwamba katika fasihi hii inabainisha uwezekano wa hadithi fupi kuwa simulizi au andishi.
Wamitila (2004) Hadithi fupi ni hadithi inayojifunga kwa idadi ndogo ya wahusika wa tukio fulani maalumu inayoonesha mabadiliko katika sehemu na wakati wa matukio au mandhari kwa upana na isiyojiingiza kwenye undani wa wahusika. Hadithi fupi husomeka kwa kipindi kifupi sana.
Kwa ujumla tunaweza kusema kwamba, hadithi fupi andishi ni aina ya kazi andishi ambayo huwa fupi na huangazia wazo moja kwa moja kwa kurejea kisa kimoja. Huwa na wahusika wachache na huchukuwa mda mfupi.
Pia wataalamu mbalimbali wamejjadili (fasili) maana ya riwaya.
Wamitila (2003) anasema, riwaya ni kazi ya kinathari au kibunilizi ambayo huwa na urefu wa kutosha, msuko uliojengeka vizuri wahusika wengi walioendelezwa kwa kina yenye kuchukuwa muda mwingi katika maandalizi kuhusisha mandhri maalumu.
Muhando na Balsidya, Riwaya ni kazi ya kubuni, ni hadithi ambayo hutungwa kufuatana na uwezo wa fanani kuibusha mambo kutokana na mazoea au mazingira yake. Wanaendelea kusema riwaya huanzia maneno elfu thelathini na tano na kuendelea.
Senkoro (2011) anasema, kuwa riwaya kiswahili zilizuka kutokana na maendeleo na mageuzi ya kiutamaduni, uchangamano wa maisha ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni yalipelekea haja ya kimaudhui zaidi ya ngano na hadithi fupi.
Madumilla (2009) anasema, Riwaya ya kiswahili ilitokana na nathari bunifu simulizi kama vile hadithi, hekana na ngano iliyosimuliwa kwa mdomo.
Kwa ujumla riwaya ya kiswahili ni ile ambayo inafungamana na utamaduni wa jamii ya waswahili wenyewe. Mwanzoni riwaya zilitafsiriwa kwa kiswahili kutoka lugha za kigeni kanma vile kiarabu na kizungu na kufanya riwaya za kiswahili kutokea mfano mfano wa riwaya hizo ni kama vile; Habari za mlima  iliyoandikwa na Shekhe Alibin Hemed (1980)
Sifa za hadithi fupi andishi na riwaya ya kiswahili:-
Hadithi fupi andishi huwa na sifa mbalimbali kama vile, kuwa na wahusika wachache na hawaelezwi kiundani, huwa na maneno machache kuanzia elfu kumi na kuendelea, huwa na kisa kimoja, pia wahusika wake huwa hawatukuzwi, suala la muktadha huwa halipewi kipaombele, na vile vile huwa na matukio machache.
Pa riwaya ya kiswahili huwa na sifa mbalimbali kama vile, masimulizi ya kubuni, huwa na sifa ya uganizi, huwa na urefu wa maneno kuanzia elfu thelathini na tano na kuendelea, pia huwa na mawanda mapana katika vipengele kama vile mandhari, wahusika,lugha na pia huwa na uchangamano kwenye visa, matukio na wahusika.
Chimbuko la hadithi fupi andishi na riwaya ya kiswahili zimechangiwa sana na fani za kijadi kama ngano, sira, tendi, masimulizi ya wasafiri, hekaya n.k na mazingira ya jamii.
Fani za kijadi zilikuwepo kwenye fasihi simulizi na kuanza kuigwa na watunzi mbalimbali kutokana na mabadiliko ya kijamii katika kufikia karne ya 16 zilizagaa kila sehemu.
Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia na maendeleo ya kiuchumi na ndipo riwaya ya kiswahili na hadithi fupi na zilipoanza.
mfano: Hadithi fupi-siku ya mganga
                                -Ngome ya nafsi
                                -Hadili na nduguye
Mfano wa Hadithi fupi:-
MSAFIRI NA NGAMIA
Msafiri mmoja aliamua kupumzika kutokana na upepo mkali na vumbi la jangwani. Aliamua kukaa ndani ya hema lake hadi hali hiyo ya hewa ibadilike ndipo aendelee na safari yake.
Ngamia wake pale nje alikumbwa na baridi kali hivyo akaamua kuomba hifadhi ndani ya hema la bwana wake. “Bwana nakuomba uniruhusu nitie kichwa changu ndani ya hema nijiepushe na athari za upepo na mavumbi yalioko hapa nje” yule msafiri alikataa na kumweleza kuwa haingewezekana kwani hema lilikuwa dogo lakini Ngamia alimrairai hadi alipokubali.
Ngamia kuona kuwa kichwa chake kiko ndani aliomba aingize shingo yake, akadai shingo yake haitachukuwa nafasi kubwa. Naye msafiri akakubali baadaye akakubaliwa kuingiza hadi nundu yake na hatimaye akaingia wote mzima. Msafiri akatabahi, alikuwa amerushwa nje huku ngamia akidai kuwa wasingeweza kuenea pamoja kwani hema lilikuwa dogo. Basi msafiri akaumia nje huku baridi inamzizima ingawa hema lilikuwa lake.
Hali ya hewa ilipobadilika msafiri alimwambia Ngamia kuwa wangeendelea na safari. Baada ya siku kadhaahali ya hewa ilibadilika, mvua kubwa ikanyesha naye msafiri akatafuta hifadhi ndani ya hema lake licha ya kuwa Ngamia alimbembeleza angalau ajiepushe na baridi. Msafiri alikuwa ameapa kutorudia kosa lake la awali.
Ufuatao ni mlinganisho kati ya hadithi fupi andishi na riwaya ya kiswahili kama ifutavyo:-
Ubunifu; zote ni fani za kubuni hubuniwa makusudi kabisa na mtunzi binafsi ambaye huisanifu na kupanga hadithi yake kwa namna anayotaka mwenyewe. Mfano wa hadithi ya “Msafiri na Ngamia” ni kisa cha kubuniwa na cha kupangwa na kusanifiwa na mtunzi kwa mawazo yake mwenyewe, pia katika riwaya ya kiswahili kama vile “Mfadhili” iliyoandikwa na “Hussen Tuwa” kisa chake ni cha kubuniwa kwani mwandishi ametunga kisa chake kutokana na uhalisia wa jamii yake.
Uhalisia; zote husawiri jamii kama ilivyo mfano katika hadithi ya “Msafiri na Ngamia” imeonekana jinsi mtu anavyopata matatizo kutokana na ukarimu mfano wakoloni walitutawala lakini tuliwakaribisha wenyewe, pia katika riwaya “Mfadhili” imeakisi jamii katika masuala ya mapenzi, ulevi, usaliti. Hivyo basi riwaya ya kiswahili na hadithi fupi andishi zote hulenga uhalisia wa jamii.
Lugha; zote hutumia lugha ya kinathari katika kisa cha Ngamia na Msafiri kimetumia lugha ya mafumbo mfano, Ngamia akimaanisha wageni waliokuja Afrika wakaomba kushirikiana na sisi lakini walipokaribishwa walibadilika na kutuletea matatizo. Msafiri, hawa ni waafrika ambao wamekaribisha wageni (wakoloni). Katika riwaya ya kiswahili (Mfadhili) imejaa tamathali za semi, mafumbo, misemo na nahau, lugha ya picha, Tashbiha mfano “gari liliruka juu kama jiwe”
Msuko; hadithi fupi andishi na riwaya ya kiswahili zote huwa wa matukio uliopangwa kwa namna yenye kuleta mtiririko wa mshikamano wa simulio zima mfano katika kisa kizima cha “Ngamia na Msafiri” kisa kimepangwa kwa mtiririko wenye kuleta mshikamano kuanzia msafiri alipomkaribisha Ngamia hadi msafiri alipofukuzwa kwenye hema lake na kukosa hifadhi. Pia katika riwaya ya mfadhili inaonesha mtiririko mzuri uliosukwa kwa visa na matukio mfano kuanzia mahusiano kati ya Gaddi Bullah na Dania kumuomba Gaddi Bullah msamaha kwani aliweza kumfadhili ini lake, hivyo inaonesha msuko na mtiriko wa tukio zima tangia mwanzo wake hadi hatima yake.
Pia upo mlinganuo uliopo kati ya hadithi fupi andishi na riwaya ya kiswahili kama ifuatavyo:-
Urefu; hadithi fupi andishi kawaida huwa haizidi maneno elfu kumi lakini riwaya ya kiswahili huwa na maneno yasiyopungua elfu thelathini na tano na kuendelea hii ni kwa sababu riwaya huwa na kisa kirefu chenye uhitaji wa maneno mengi na wahusika wengi ili kukamilisha kisa kizima ukilinganisha na hadithi fupi andishi kisa chake ni kifupi hivyo huhitaji pia maneno machache kukamilisha simulizi zima.
Uchangamano; hadithi fupi andishi huwa na muundo sahili usiyochangamana na uliyo na tukio moja tu, mfano katika kisa cha “ Ngamia na Msafiri” tunaona tukio linalozungumziwa ni moja linalomhusu Ngamia na Msafiri hivyo huwa ni muundo wa moja kwa moja lakini katika riwaya ya “Mfadhili” ina muundo changamano kwani hueleza kisa cha Dania na Gadi Bullah.
Wahusika; hawa ni watu, vitu na mahali na miungu katika kazi ya fasihi, katika hadithi fupi andishi huwa na wahusika wachache angalabu mhusika mkuu huwa ni mmoja au wawili na wahusika huwa hawakui tabia zao hudhihirika kutokana na matukio mfano katika hadithi fupi ya “ Ngamia na Msafiri” tunaona kuwa wahusika wawili tu katika kisa kizima lakini katika riwaya ya kiswahili wahusika wanakuwa ni wengi, wahusika wakuu huwa ni zaidi ya wawili na pia wahusika hukua,tabia zao hujenga na husababisha matukio, huwa na wahusika wakuu na wajenzi mfano katika riwaya ya “Mfadili” wahusika wakuu ni Gadi Bullah na Dania na wahusika wengine wajenzi.
Dhamira; hapa tunaona kuwa hadithi fupi andishi huwa na dhamira chache aghalabu dhamira kuu moja Mfano katika hadithi hii ya “Ngamia na Msafiri” wazo kuu ni unyonyaji lakini riwaya ya kiswahili huwa na dhamira kuu na dhamira ndogondogo zinazosaidia kukamilisha wazo kuu mfano katika riwaya ya “Mfadhili” dhamira kuu ni “ Mapenzi na ndoa” na dhamira ndogondogo ni kama vile ulevi, usaliti,, bidii katika kazi na ufanisi, ukarimu hivo dhamira hizi ndogondogo husaidia wazo kuu ili kukamilisha simulizi zima.
Mandhari, hili ni eneo au mahali tukio la kazi ya fasihi simulizi au andishi hufanyika, katika hadithi fupi andishi mandhari huwa na mawanda finyu kiwakati wa kijiografia mfano katika hadithi ya “Msafiri na Ngamia” Mandhari iliyotumika ni ya jangwani mahali alipokuwa amejenga hema lake Msafiri lakini katika riwaya ya kiswahili huwa na mawanda  mapana kiwakati na kijiografia, mfano katika riwaya ya “Mfadhili” mandhari iliyotumika ni ya hotelini, Zanzibar, Arusha na Dar es salaam hivyo huonesha mawanda mapana sana ukilinganisha na mandhari ya hadithi fupi andishi.
Japokuwa kuna utofauti uliopo kati ya riwaya ya kiswahili na hadithi fupi andishi lakini zote zinalenga kuelimisha jamii kwani zote zinazungumzia masuala ya jamii husika kama vile mapenzi na ndoa, usaliti, ulevi na dhuluma na pia riwaya ya kiswahili na hadithi fupi andishi zote zinajikita katika kutoa mafunzo na maadili na pia zinatoa masuluhisho mbalimbali ya migogoro inayoikumba jamii, hususani katika migogoro ya kiuchumi kisiasa na kijamii


MAREJEO
Madumulla J.S (2009), Riwaya ya kiswahili na misingi ya uchambuzi,Nairobi:Sitima printer Ltd.
Mulokozi M.M (1996), Utangulizi wa fasihi ya kiswahili, Dar es salaam: TUKI.
Msokole M.(1992), Misingi ya hadithi fupi, Dar es salaam: Dar es salaam University press.
Samwel M,(2012), Hadithi fupi, Nadharia, Mbinu na mifano, Dodoma: Kusenyanda Tanzania.

Hakiki riwaya ya Mirathi ya Hatari au Kurwa na Doto kwa kuzingatia misingi ya falsafa ya kiafrika ya Placide Tempels. mawazo haya yana nafasi gani katika jamii ya leo ya kitanzania.


Maana ya falsafa ya kiafrika kwa mujibu wa Placide Tempels, Falsafa ya kiafrika ni ile falsafa inayowashughulisha waafrika wenyewe na watu wengine ambao sio waafrika lakini wanakubaliana na mila, tamaduni za waafrika na fasihi simulizi za kiafrika.Hivyo falsafa ya kiafrika ni ile falsafa ambayo imejikita katika mifumo ya kijamii, mila na desturi na fasihi simulizi za kiafrika.
Placide Tempels alizaliwa tarehe 18/02/1906 katika mji wa Barcal huko Ubelgiji na alikufa tarehe 09/10/1977 akiwa na umri wa miaka sabini na moja huko huko Ubelgiji. Aliishi Kongo kwa miaka ishirini na tisa mpaka pale aliporejea kwao ubelgiji.  Kwa kipindi chote alipokuwa Kongo alifanya kazi kuu mbili, kazi ya umishenari na uandishi.Katika kipindi chote hicho alichokaa Kongo alisoma tabia ya waafrika wanaoishi Kongo hususani kabila la Waruba, na akabaini kuwa waafrika wana tamaduni zao zilizojikita katika fasihi simulizi. Hivyo akaandika kitabu chake kiitwacho “The Bantu philosophy” (1945), katika kitabu hicho anapinga mawazo ya wazungu kwa kusema kuwa waafrika wanafalsafa yao na hivyo Tempels akatumia hoja kadhaa kutetea mawazo yake hayo, kama imani ya uchawi, hofu ya uhai na kifo, nguvu hai, suala la ndoa na dhana ya uduara.
Katika kujibu swali hili riwaya ya “Mirathi ya Hatari” ndio inayotumika. “Mirathi ya Hatari” ni riwaya ilioandikwa na C. G. Mung’ong’o (1977). Riwaya hii inajaribu kuelezea visa na mikasa ya kisihiri iliojitokeza katika jamii za kiafrika hususani katika jamii ya Njombe (Kiterevadzi) na maeneo mengine. Hivyo msanii amemtumia mhusika Gusto ambaye ndiye anayerithishwa mirathi ya hatari kutoka kwa baba yake Mzee Kazembe, mirathi hiyo ndiyo inayopelekea vifo vingi kutokea ikiwemo visasi mfano kifo cha mama yake Gusto na dada yake Nandi, pia inapelekea kifo cha mjomba ake Gusto Kapedzile. Ukiachana na vifo hivyo pia inapelekea kutokea kwa matukio mengi ya kiuchawi.
Ufuatao ni uhakiki wa riwaya ya “Mirathi ya hatari” kwa kuzingatia misingi ya kisalsafa kama ilivyoainishwa na Placide Tempels katika kitabu cha “The Bantu Philosophy” na kuonyesha uhalisia wake na faida na hasara ya falsafa hiyo katika jamii ya kitanzania.
Imani ya uchawi, Katika falsafa ya imani ya uchawi Tempels anaamini kwamba waafrika wanategemea sana nguvu za kichawi, katika kuelezea suala hilo Tempels anajaribu kuangalia jamii ya Ulaya kwamba wengi wapatapo matatizo hurudi kwa Kristo lakini jamii nyingi za Afrika pindi wapatapo matatizo hutegemea uchawi kama suluhisho la matatizo yao wanayarudisha kwenye imani za kishirikina. Falsafa hii ya imani ya uchawi imejitokeza kwa kiasi kikubwa sana katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari” kwani kuna matukio mengi ambayo yanadhihirisha hilo. Mfano,  kitendo cha Gusto kukabidhiwa mirathi ya uchawi kutoka kwa baba yake. Mfano uk. 15 Mzee Kazembe anamwambia Gusto “Mwanangu nakuachia kazi kubwa. Ni urithi mkubwa ukiutumia vyema, bali pia ni mirathi ya hatari usipojihadhari nayo, nakuachia dawa zote za milki yangu katika mizungu ya sihiri”. Pia uwepo wa kiapo cha uchawi, unadhihilika pale ambapo Gusto anaapishwa kama ni uaminifu wa kuingia katika uchawi kiapo hicho kila mtu anahitaji kiapo ndipo awe mchawi; mfano katika ukurasa wa 21 anaonekana akiapa kwa kutamka maneno, “Enyi Mahoka na Mababu...”. Pia mazingira ya vifo vyote, vinatokea katika mazingira ya utatanishi ambayo ni mazingira ya kichawi. Mfano, kifo cha Kapedzile, ambaye aliuliwa na Gusto, kifo cha Dina ambaye aliuliwa katika mazingira ya kichawi na baba yake, kifo cha mama yake Gusto Nyamidze na Nandi ambao walikuwa na Malipula kwa kutaka kulipa kisasi na kifo cha Malipula aliyeuliwa na Gusto pamoja na Mavengi katika mazingira ya Kichawi.
Katika jamii yetu ya kitanzania imani ya uchawi inajitokeza sana kwani kuna matukio mengi yanayojitokeza na yanaonekana kiuhalisia mfano watu kugandishwa katika nyumba za watu na pia kila kukicha wanaonekana wakianguka usiku na Nyungo zao, pia suala la uwepo wa misukule katika nyumba za watu. Pia baadhi ya watu kutumia hirizi kama kinga. Falsafa ya imani ya kichawi haina nafasi katika jamii kwani inasababisha migogoro mingi, maafa pamoja na kurudisha maendeleo nyuma. Hivyo wanajamii wa leo wanaaswa kuachana na imani za kichawi.
Hofu ya uhai na kifo. Hii ni hoja nyingine ya Tempels kwani anaamini kuwa Waafrika wana hofu ya uhai na kifo. Kwa kudhihilisha hili anaweza kuangalia salamu zao, na pia mtu anapopatwa na ugonjwa anaamini hawezi kupona na kifo kinamsogelea. Wazo hili limejitokeza pia katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari” mfano pale Mzee Kazembe anapomueleza mwanae kuwa hali yake ni mbaya na kifo kinamkaribia uk. 15 “Siku zangu zimekwisha sidhani kama nitaishi zaidi”. Pia mama yake Gusto alikuwa na hofu na uhai wa Gusto na ndio maana akamuusia aachane na mirathi aliyokabidhiwa na baba yake kwani anaweza akapoteza maisha. uk 38 “Sipendi nimpoteze tena hata mmoja wenu kabla sijafa”.Pia suala la salamu na kujua hali ya mtu inaonesha hofu ya kifo, mfano ni pale Malipula alipokwenda nyumbani kwa kina Gusto walianza kujuliana hali uk. 57,......Nikawauliza....., “Habari za nyumbani wazee wangu”, “Nyumbani kwema tu” alijibu mzee Kindimba “Lakini hatujui ya huko nyuma”
Suala la hofu ya uhai na kifo linajitokeza sana katika jamii ya kitanzania mfano, Watanzania asubuhi wakiamka au wasipoonana muda mrefu basi hutoleana salamu na kujuliana hali, pia pale mtu anapoamua watu huwa na wasiwasi sana na uhai wake hivyo hujikithirisha kumuombea dua ili aweze kupona. Falsafa ya uhai na kifo ina nafasi katika jamii kwani inawafanya wanajamii kuchukuwa tahadhari ili kuzuia kifo, pia inaendeleza dhana ya kustawisha zaidi uhai. Kwa upande mwingine falsafa hii in hasara kwani hurudisha nyuma maendeleo kwa sababu mtu ataogopa kufanya suala la maendeleo kwa kuhofia kifo ambacho kitamfanya kuacha mali zote alizochuma pia kutotimiza malengo yake.
Waafrika wanaamini katika suala la ndoa, pia hili ni wazo la Placide Tempels ambae anasema kuwa waafrika wanaamini sana katika ndoa zao na ndoa hizo hudumishwa ili kupata watoto. Uhai wa binadamu unaanzia kwenye mimba ambayo ni matokeo ya Ndoa. Wazo hili linaonekana sana katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari” mfano ndoa ya Kazembe na Nyamidze watoto wanaopatikana ni nane na wanaokufa ni watoto watano ambapo uk. 5 unaonyesha hilo. Pia  familia ya Malipula na mkewe pia wana watoto. Pia mjomba wake Dina alikuwa na ndoa iliyompeleka kupata watoto katika uk.78.
Suala hili la ndoa linasawiri maisha halisi ya kila siku ya Tanzania mfano kuna ndoa za kanisani, msikitini ndoa za serikali na ndoa za kijadi. Suala la ndoa lina nafasi kubwa katika jamii kwani inaendeleza nguvu kazi inayotokana na watoto wanaozaliwa ambao wanatumika katika ujenzi wa taifa kwa sababu hujishughulisha na shughulu mbalimbali  za ujenzi wa taifa. Pia falsafa hii huunganisha jamii, vile vile inaleta heshima katika jamii. Kwa upande wa hasara ni pale inapotokea ndoa za kulazimishwa au umri mdogo, kwani kuna wazazi wanawazoesha watoto wao wakiwa bado wanafunzi.
Waafrika wanaamini katika nguvu hai, hili ni wazo jingine la Tempels kwani anasema kwamba waafrika wanaamini sana katika nguvu hai na wanaamini kwamba chanzo kikuu cha nguvu hai ni Mungu mwenyewe, nguvu hii hupitia kwa wahenga nao hupeleka kwa mizimu ambao hupeleka kwa binadamu na binadamu hupeleka kwa wanyama na mimea. Tempels anasema waafrika wanaamini nguvu ya waganga na hivyo mganga ana uwezo mkubwa wa kupunguza au wakuongeza nguvu hai kwa binadamu. Tempels anajiuliza maswali kadhaa kuhusiana na suala la waganga mfano, Dawa zawezaje kuponya?, Dawa inawezaje kuua mtu aliye mbali?, ni vipi mtu aliyekufa anaweza kuzaliwa upya?,na anasema kitendo cha kupungukiwa nguvu huitwa “Kufwa” na “Kufudwilika” katika ukurasa wa 22. Hivyo Tempels anasema kuwa majibu ya maswali yote matatu, ili uweze kujibu maswali hayo ni lazima uwe mshirika wa mambo hayo. Dhana hii inajitokeza katika riwaya ya  “Mirathi ya Hatari” mfano baada ya kufa Mzee Kazembe mke wake Nyamidze alikwenda kwa mganga kuthibitisha nini hasa chanzo cha kifo hicho uk.37. “Mwanangu leo asubuhi nilikwenda kwa mama Tamwene kuulizia kifo cha baba yako. Mganga anasema kuwa kifo chake kimetokea si kwa mapenzi ya Mungu ila kwa michezo ya binadamu wafaidio kuwaona watu wakifa” Mama Gusto alimwambia mwanawe Gusto. Pia Malipula alitaka ampeleke Gusto kwa Chikanga (Mganga) ili kubaini kama amehusika  na mauaji ya Kapedzile katika uk.60.
Jambo hili katika jamii ya sasa bado linaendelea, kwani Watanzania wengi huenda kwa waganga ili kukamilisha mambo yao, mfano kwenye masuala ya siasa, elimu, biashara, kilimo, mauaji ya albino, upigaji wa nondo, uchunaji wa ngozi yote haya yanahusishwa na waganga. Falsafa hii ina nafasi katika jamii kwani inaendeleza uhai pale mwanadamu anapojihangaisha na kutafuta tiba ya maradhi yake na hatimae anaweza kupona na kuendelea kuishi. Pia imani hii ya ya nguvu hai inaweza kupelekea migogoro katika jamii hasa waganga wa jadi wanaposhirikishwa katika kuongeza nguvu hata pamoja na kupiga ramli huzusha mgogoro katika jamii.
Dhana ya uduara, katika wazo hili Tempels anasema kuwa waafrika hupenda vitu vya umbo la uduara kwani wanaamini kuwa hivyo ndivyo vitu vizuri. Mfano katika riwaya ya “Mirathi ya Hatari” dhana hii inaonekana sehemu nyingi. Mfano, pale Gusto alipoingizwa kwenye pango na kukalishwa katika kigoda chenye umbo la duara katika ukurasa wa 33. Pia Gusto anapomsifia Dina kuwa ana uso wa mviringo katika ukurasa wa 30. Vile vile Mavengi anapoupitisha mgwisho wake na kuwazungushia Dina na Gusto katika umbo la duara uk.73. Hata meza ya Gusto ilikuwa ni ya mviringo.
Dhana hii inajitokeza katika jamii ya leo mfano nyumba za msonge katika kanda ya ziwa, Mikao ya kula huwa katika duara pia vyombo vingi huwa na umbo la duara kama sufuria ,Vyungu, Vinu, Nyungo za kupepetea na Ngoma. Falsafa ya uduara ina nafasi katika jamii kwani hudumisha na kuendeleza utamaduni wa mwafrika, kwani tangu zamani inaaminika kuwa kila kitu chenye uduara ni kizuri, pia kuna jamii nyingine zinazoendeleza kujenga nyumba za msonge. Hasara ya falsafa hii hushirikisha imani hii ya uduara kama ndiyo kitu pekee kizuri, kwani kuna vitu vingine ambavyo si duara na ni vizuri.
Kwa ujumla Placide Tempels ametoa mchango mkubwa sana juu ya falsafa ya kiafrika, ambaye anakubali kabisa kuwa waafrika wana falsafa yao. Mawazo yake yanapelekea kuibuka kwa wanafalsafa wengine wanaoizungumzia falsafa ya kiafrika kama vile Kwame Nkurumah, J. K. Nyerere, Kenneth Kaunda. Hivyo basi mawazo yake yana uhalisia pia yana umuhimu katika jamii ya kiafrika.





MAREJEO
Mung’ong’o C. G. (1977), Mirathi ya Hatari. Dar es salaam: Tanzania Publisha House.
Tempels, P, (1959),The Bantu Philosophy. Paris: Presence Africaine.