Wataalamu mbalimbali wametoa fasili mbalimbali za hadithi
fupi andishi kama ifuatavyo:-
Msokile (1992) Anasema, hadithi fupi ni aina ya kazi ya
sanaa ya utanzu wa hadithi inayotumia lugha iliyoandikwa katika nathari au
iliyo katika masimulizi kama haijaandikwa. Ni wazi kwamba katika fasihi hii
inabainisha uwezekano wa hadithi fupi kuwa simulizi au andishi.
Wamitila (2004) Hadithi fupi ni hadithi inayojifunga kwa
idadi ndogo ya wahusika wa tukio fulani maalumu inayoonesha mabadiliko katika
sehemu na wakati wa matukio au mandhari kwa upana na isiyojiingiza kwenye
undani wa wahusika. Hadithi fupi husomeka kwa kipindi kifupi sana.
Kwa ujumla tunaweza kusema kwamba, hadithi fupi andishi
ni aina ya kazi andishi ambayo huwa fupi na huangazia wazo moja kwa moja kwa
kurejea kisa kimoja. Huwa na wahusika wachache na huchukuwa mda mfupi.
Pia wataalamu mbalimbali wamejjadili (fasili) maana ya
riwaya.
Wamitila (2003) anasema, riwaya ni kazi ya kinathari au
kibunilizi ambayo huwa na urefu wa kutosha, msuko uliojengeka vizuri wahusika
wengi walioendelezwa kwa kina yenye kuchukuwa muda mwingi katika maandalizi
kuhusisha mandhri maalumu.
Muhando na Balsidya, Riwaya ni kazi ya kubuni, ni hadithi
ambayo hutungwa kufuatana na uwezo wa fanani kuibusha mambo kutokana na mazoea
au mazingira yake. Wanaendelea kusema riwaya huanzia maneno elfu thelathini na
tano na kuendelea.
Senkoro (2011) anasema, kuwa riwaya kiswahili zilizuka
kutokana na maendeleo na mageuzi ya kiutamaduni, uchangamano wa maisha ya
kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni yalipelekea haja ya kimaudhui zaidi
ya ngano na hadithi fupi.
Madumilla (2009) anasema, Riwaya ya kiswahili ilitokana
na nathari bunifu simulizi kama vile hadithi, hekana na ngano iliyosimuliwa kwa
mdomo.
Kwa ujumla riwaya ya kiswahili ni ile ambayo inafungamana
na utamaduni wa jamii ya waswahili wenyewe. Mwanzoni riwaya zilitafsiriwa kwa
kiswahili kutoka lugha za kigeni kanma vile kiarabu na kizungu na kufanya
riwaya za kiswahili kutokea mfano mfano wa riwaya hizo ni kama vile; Habari za
mlima iliyoandikwa na Shekhe Alibin
Hemed (1980)
Sifa za hadithi fupi andishi na riwaya ya kiswahili:-
Hadithi fupi andishi huwa na sifa mbalimbali kama vile,
kuwa na wahusika wachache na hawaelezwi kiundani, huwa na maneno machache
kuanzia elfu kumi na kuendelea, huwa na kisa kimoja, pia wahusika wake huwa
hawatukuzwi, suala la muktadha huwa halipewi kipaombele, na vile vile huwa na
matukio machache.
Pa riwaya ya kiswahili huwa na sifa mbalimbali kama vile,
masimulizi ya kubuni, huwa na sifa ya uganizi, huwa na urefu wa maneno kuanzia
elfu thelathini na tano na kuendelea, pia huwa na mawanda mapana katika
vipengele kama vile mandhari, wahusika,lugha na pia huwa na uchangamano kwenye
visa, matukio na wahusika.
Chimbuko la hadithi fupi andishi na riwaya ya kiswahili zimechangiwa
sana na fani za kijadi kama ngano, sira, tendi, masimulizi ya wasafiri, hekaya
n.k na mazingira ya jamii.
Fani za kijadi zilikuwepo kwenye fasihi simulizi na
kuanza kuigwa na watunzi mbalimbali kutokana na mabadiliko ya kijamii katika
kufikia karne ya 16 zilizagaa kila sehemu.
Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia na
maendeleo ya kiuchumi na ndipo riwaya ya kiswahili na hadithi fupi na
zilipoanza.
mfano: Hadithi fupi-siku ya mganga
-Ngome ya nafsi
-Hadili na nduguye
Mfano wa Hadithi fupi:-
MSAFIRI NA NGAMIA
Msafiri mmoja aliamua kupumzika kutokana na upepo mkali
na vumbi la jangwani. Aliamua kukaa ndani ya hema lake hadi hali hiyo ya hewa
ibadilike ndipo aendelee na safari yake.
Ngamia wake pale nje alikumbwa na baridi kali hivyo
akaamua kuomba hifadhi ndani ya hema la bwana wake. “Bwana nakuomba uniruhusu
nitie kichwa changu ndani ya hema nijiepushe na athari za upepo na mavumbi
yalioko hapa nje” yule msafiri alikataa na kumweleza kuwa haingewezekana kwani
hema lilikuwa dogo lakini Ngamia alimrairai hadi alipokubali.
Ngamia kuona kuwa kichwa chake kiko ndani aliomba aingize
shingo yake, akadai shingo yake haitachukuwa nafasi kubwa. Naye msafiri
akakubali baadaye akakubaliwa kuingiza hadi nundu yake na hatimaye akaingia
wote mzima. Msafiri akatabahi, alikuwa amerushwa nje huku ngamia akidai kuwa
wasingeweza kuenea pamoja kwani hema lilikuwa dogo. Basi msafiri akaumia nje
huku baridi inamzizima ingawa hema lilikuwa lake.
Hali ya hewa ilipobadilika msafiri alimwambia Ngamia kuwa
wangeendelea na safari. Baada ya siku kadhaahali ya hewa ilibadilika, mvua
kubwa ikanyesha naye msafiri akatafuta hifadhi ndani ya hema lake licha ya kuwa
Ngamia alimbembeleza angalau ajiepushe na baridi. Msafiri alikuwa ameapa
kutorudia kosa lake la awali.
Ufuatao ni mlinganisho kati ya hadithi fupi andishi na
riwaya ya kiswahili kama ifutavyo:-
Ubunifu; zote ni fani za kubuni hubuniwa makusudi kabisa
na mtunzi binafsi ambaye huisanifu na kupanga hadithi yake kwa namna anayotaka
mwenyewe. Mfano wa hadithi ya “Msafiri na Ngamia” ni kisa cha kubuniwa na cha
kupangwa na kusanifiwa na mtunzi kwa mawazo yake mwenyewe, pia katika riwaya ya
kiswahili kama vile “Mfadhili” iliyoandikwa na “Hussen Tuwa” kisa chake ni cha
kubuniwa kwani mwandishi ametunga kisa chake kutokana na uhalisia wa jamii
yake.
Uhalisia; zote husawiri jamii kama ilivyo mfano katika
hadithi ya “Msafiri na Ngamia” imeonekana jinsi mtu anavyopata matatizo
kutokana na ukarimu mfano wakoloni walitutawala lakini tuliwakaribisha wenyewe,
pia katika riwaya “Mfadhili” imeakisi jamii katika masuala ya mapenzi, ulevi,
usaliti. Hivyo basi riwaya ya kiswahili na hadithi fupi andishi zote hulenga
uhalisia wa jamii.
Lugha; zote hutumia lugha ya kinathari katika kisa cha
Ngamia na Msafiri kimetumia lugha ya mafumbo mfano, Ngamia akimaanisha wageni
waliokuja Afrika wakaomba kushirikiana na sisi lakini walipokaribishwa
walibadilika na kutuletea matatizo. Msafiri, hawa ni waafrika ambao
wamekaribisha wageni (wakoloni). Katika riwaya ya kiswahili (Mfadhili) imejaa
tamathali za semi, mafumbo, misemo na nahau, lugha ya picha, Tashbiha mfano
“gari liliruka juu kama jiwe”
Msuko; hadithi fupi andishi na riwaya ya kiswahili zote
huwa wa matukio uliopangwa kwa namna yenye kuleta mtiririko wa mshikamano wa
simulio zima mfano katika kisa kizima cha “Ngamia na Msafiri” kisa kimepangwa
kwa mtiririko wenye kuleta mshikamano kuanzia msafiri alipomkaribisha Ngamia
hadi msafiri alipofukuzwa kwenye hema lake na kukosa hifadhi. Pia katika riwaya
ya mfadhili inaonesha mtiririko mzuri uliosukwa kwa visa na matukio mfano
kuanzia mahusiano kati ya Gaddi Bullah na Dania kumuomba Gaddi Bullah msamaha
kwani aliweza kumfadhili ini lake, hivyo inaonesha msuko na mtiriko wa tukio
zima tangia mwanzo wake hadi hatima yake.
Pia upo mlinganuo uliopo kati ya hadithi fupi andishi na
riwaya ya kiswahili kama ifuatavyo:-
Urefu; hadithi fupi andishi kawaida huwa haizidi maneno
elfu kumi lakini riwaya ya kiswahili huwa na maneno yasiyopungua elfu
thelathini na tano na kuendelea hii ni kwa sababu riwaya huwa na kisa kirefu
chenye uhitaji wa maneno mengi na wahusika wengi ili kukamilisha kisa kizima
ukilinganisha na hadithi fupi andishi kisa chake ni kifupi hivyo huhitaji pia
maneno machache kukamilisha simulizi zima.
Uchangamano; hadithi fupi andishi huwa na muundo sahili
usiyochangamana na uliyo na tukio moja tu, mfano katika kisa cha “ Ngamia na
Msafiri” tunaona tukio linalozungumziwa ni moja linalomhusu Ngamia na Msafiri
hivyo huwa ni muundo wa moja kwa moja lakini katika riwaya ya “Mfadhili” ina
muundo changamano kwani hueleza kisa cha Dania na Gadi Bullah.
Wahusika; hawa ni watu, vitu na mahali na miungu katika
kazi ya fasihi, katika hadithi fupi andishi huwa na wahusika wachache angalabu
mhusika mkuu huwa ni mmoja au wawili na wahusika huwa hawakui tabia zao
hudhihirika kutokana na matukio mfano katika hadithi fupi ya “ Ngamia na
Msafiri” tunaona kuwa wahusika wawili tu katika kisa kizima lakini katika
riwaya ya kiswahili wahusika wanakuwa ni wengi, wahusika wakuu huwa ni zaidi ya
wawili na pia wahusika hukua,tabia zao hujenga na husababisha matukio, huwa na
wahusika wakuu na wajenzi mfano katika riwaya ya “Mfadili” wahusika wakuu ni
Gadi Bullah na Dania na wahusika wengine wajenzi.
Dhamira; hapa tunaona kuwa hadithi fupi andishi huwa na
dhamira chache aghalabu dhamira kuu moja Mfano katika hadithi hii ya “Ngamia na
Msafiri” wazo kuu ni unyonyaji lakini riwaya ya kiswahili huwa na dhamira kuu
na dhamira ndogondogo zinazosaidia kukamilisha wazo kuu mfano katika riwaya ya
“Mfadhili” dhamira kuu ni “ Mapenzi na ndoa” na dhamira ndogondogo ni kama vile
ulevi, usaliti,, bidii katika kazi na ufanisi, ukarimu hivo dhamira hizi
ndogondogo husaidia wazo kuu ili kukamilisha simulizi zima.
Mandhari, hili ni eneo au mahali tukio la kazi ya fasihi
simulizi au andishi hufanyika, katika hadithi fupi andishi mandhari huwa na
mawanda finyu kiwakati wa kijiografia mfano katika hadithi ya “Msafiri na
Ngamia” Mandhari iliyotumika ni ya jangwani mahali alipokuwa amejenga hema lake
Msafiri lakini katika riwaya ya kiswahili huwa na mawanda mapana kiwakati na kijiografia, mfano katika
riwaya ya “Mfadhili” mandhari iliyotumika ni ya hotelini, Zanzibar, Arusha na
Dar es salaam hivyo huonesha mawanda mapana sana ukilinganisha na mandhari ya
hadithi fupi andishi.
Japokuwa kuna utofauti uliopo kati ya riwaya ya kiswahili
na hadithi fupi andishi lakini zote zinalenga kuelimisha jamii kwani zote
zinazungumzia masuala ya jamii husika kama vile mapenzi na ndoa, usaliti, ulevi
na dhuluma na pia riwaya ya kiswahili na hadithi fupi andishi zote zinajikita
katika kutoa mafunzo na maadili na pia zinatoa masuluhisho mbalimbali ya
migogoro inayoikumba jamii, hususani katika migogoro ya kiuchumi kisiasa na
kijamii
MAREJEO
Madumulla J.S (2009), Riwaya ya
kiswahili na misingi ya uchambuzi,Nairobi:Sitima printer Ltd.
Mulokozi M.M (1996), Utangulizi wa
fasihi ya kiswahili, Dar es salaam: TUKI.
Msokole M.(1992), Misingi ya hadithi
fupi, Dar es salaam: Dar es salaam University press.
Samwel M,(2012), Hadithi fupi,
Nadharia, Mbinu na mifano, Dodoma: Kusenyanda Tanzania.
No comments:
Post a Comment